Makala hii inachunguza namna waandishi wanawake wa Kiswahili wanavyojenga na kuwasilisha ubabedume (uanaume wa jadi au kibabe) kupitia wahusika wa kiume katika riwaya teule. Ingawa tafiti nyingi zimejikita katika usawiri wa wanawake ndani ya mfumo dume, nafasi ya waandishi wanawake katika kuibua na kuchambua ujenzi wa ubabedume imepewa uzito mdogo katika uhakiki wa fasihi ya Kiswahili. Kwa msingi huo, makala hii inalenga kubainisha vitambulishi vya ubabedume vinavyojitokeza katika riwaya teule na kueleza jinsi vinavyojengwa kupitia wahusika na mazingira ya kijamii wanamoishi. Makala hii imeongozwa na Nadharia ya Ubabedume ya Connell (1995) na imetumia mkabala wa kimaelezo wa uchanganuzi wa yaliyomo ya kifasihi. Data ilitokana na riwaya mbili za Kiswahili zilizoandikwa na waandishi wanawake – Yanarudia Tena (Himid, 2007) na Penzi la Damu (Manyanza, 2017), ambapo matukio, mazungumzo na tabia za wahusika wa kiume zilichanganuliwa kwa kuzingatia mihimili ya ubabedume. Matokeo yanaonyesha kuwa ubabedume hujengwa kupitia sifa kama mamlaka na udhibiti, mafanikio na hadhi ya kijamii, uthubutu na ukakamavu, kujitegemea na kutoonyesha udhaifu pamoja na jukumu la ulinzi na ukimu wa jamii. Aidha, ujenzi huu unaimarishwa na taasisi za kijamii kama familia, utamaduni na mila ambazo huendeleza matarajio maalumu kuhusu mwanaume halisi. Makala hii inahitimisha kuwa waandishi wanawake wanaitumia riwaya kama jukwaa la kufichua na kuhoji ujenzi wa ubabedume, wakionesha kuwa uanaume huo si hali ya kimaumbile bali ni zao la michakato ya kijamii na kitamaduni.